Wednesday, January 24, 2018

Serikali yasema Kuna dalili za neema ya Tanzanite siku zijazo


SERIKALI imesema mazungumzo baina yake na kampuni ya Tanzanite One kuhusu uchimbaji na biashara ya madini ya Tanzanite, yako kwenye hatua nzuri na kuna dalili za neema siku zijazo.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa jana na Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, baada ya mazungumzo na kampuni hiyo kumalizika serikali sasa itaendelea na kampuni nyingine zinazochimba madini hayo mkoani Manyara.

Kwa mujibu wa Profesa Kabudi, mazungumzo na kampuni ya Barrick ni kielelezo cha utayari wa Tanzania kukaa meza moja na kampuni za uchimbaji kujadili jinsi pande zote zinavyoweza kunufaika na rasilimali.

Majadiliano kati ya Kamati Maalum iliyoundwa na Rais John Magufuli na wawakilishi kutoka kampuni ya madini ya Barrick Gold ya Canada ya katikati ya mwaka jana yalihusu biashara ya madini yanayochimbwa na migodi ya kampuni yake tanzu ya Acacia.

"Tunawahamasisha wawekezaji waje kujenga viwanda vya kusafisha madini hapa nchini kwetu, ili kuyaongezea thamani kabla ya kuyasafirisha," alisema Prof. Kabudi.

Aidha, Waziri huyo alisema sheria mpya zimetungwa ili kurekebisha mapungufu yaliyokuwapo katika mikataba ya miaka ya nyuma.

"Sasa usuluhishi wowote wa migogoro ya masuala ya madini utafanyika nchini. Tumeshaandaa muswada wa kupeleka bungeni kwa ajili ya kutugwa sheria mpya ya usuluhishi," alifafanua.

Acacia ilipokea kutoka Mamlaka ya Mapato (TRA) hati ya madai ya jumla ya Sh. trilioni 425 mwaka jana kwa kuwa mgodi wa Acacia wa Bulyanhulu unadaiwa kodi ya tangu mwaka 2000 na Pangea unadaiwa kodi ya kati ya 2007-2017.

Taarifa ya TRA kwa Acacia mwaka jana inafuatia ripoti ya tume mbili za Rais Magufuli ambazo Mei na Juni, mwaka jana ziligundua udanganyifu mkubwa katika biashara ya makinikia ya Acacia.

Moja ya ripoti hizo ilionyesha kuwa nchi inaweza kuwa imepoteza mpaka Sh. trilioni 489 katika kodi na mali (madini) kwa miaka 19 iliyopita kwenye biashara hiyo ya madini inayofanywa na Acacia.

MARA YA KWANZAHabari njema kutoka mazungumzo na Tanzanite One zinakuja miezi mitatu tangu kwa mara ya kwanza katika historia, Wizara ya Madini kufanya mnada wa Tanzanite inayozalishwa na kampuni nne kubwa za uchimbaji na biashara ya madini hayo nchini katika eneo pekee inakopatikana duniani - Mirerani wilayani Simanjiro mkoani Manyara.

Kufanyika kwa mnada wa madini hayo Mirerani hatimaye badala ya mjini Arusha, ni moja kati ya ndoto za Rais wa tano Magufuli.

Kaimu Kamishna Msaidizi wa Uchumi na Biashara ya Madini wizarani, Godleader Shoo, alisema Oktoba 12, mwaka jana kufanya mnada Mirerani ni jitihada za Serikali za kudhibiti utoroshwaji wa madini hayo nje ya nchi na pia kusaidia wachimbaji kuuza madini yao kwa bei ya ushindani inayoendana na soko la dunia.

Akizungumza wilayani humo Septemba 20, mwaka jana, Rais Magufuli alisema ndoto yake ni kuona soko la Tanzanite linakuwa Simanjiro ili wafanyabiashara kutoka ng’ambo kama Marekani, India na Ulaya wafike kwenye eneo hilo kufanya biashara.

“(Serikalini) Tunataka soko la tanzanite linakuwa hapa Simanjiro ili hawa wafanyabiashara wafunge safari waje kununulia hapa," alisema Rais Magufuli akihutubia wakazi wa eneo hilo na mikoa ya Simanjiro, Arusha na Kilimanjaro kwa ujumla.

"Na hiyo itakuwa na manufaa pia kwa wafanyabiashara wa eneo hilo maana hata yule mchinja mbuzi ama mwenye gesti atafaidika na ujio huo.”

Rais Magufuli alikuwa akizindua barabara ya kiwango cha lami ya Njia Panda ya KIA-Mererani yenye urefu wa kilometa 26 ambayo ujenzi wake umegharimu Sh. bilioni 32.5

    Choose :
  • OR
  • To comment
No comments:
Write comments