Wednesday, January 24, 2018

Kiwango cha Simba chamkuna Djuma

KAIMU KOCHA MKUU WA TIMU HIYO, MASOUD DJUMA.

WAKATI Simba ikifanikiwa kurejea kileleni mwa msimamo wa Ligi Kuu,  kaimu kocha mkuu wa timu hiyo, Masoud Djuma, amesema kikosi cha timu hiyo kinazidi kuimarika na kazi inaonekana sasa uwanjani.

Simba inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa, juzi ilifanikiwa kupata pointi tatu baada ya kuifunga Kagera Sugar kwa mabao 2-0 huku matokeo hayo yakiwa kama ya kulipiza kisasi kwa 'Wakata Miwa' hao ambao walichangia kiasi kikubwa kuwanyima ubingwa msimu uliopita baada ya kuifunga 2-1.

Akizungumza jana, Djuma, alisema anashukuru timu yake inazidi kuimarika zaidi huku pia wakifanikiwa kuvunja historia ya hivi karibuni ya Simba kutopata ushindi mbele ya Kagera Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba.

“Nafikiri kazi inaonekana, na tunaendelea vizuri, kila mchezo mmoja unapomalizika tunaanza maandalizi ya mchezo unaofuata, tutaendelea kupambana kuhakikisha tunafikia malengo yetu,” alisema Djuma.

Alisema kwa sasa wanaelekeza nguvu zao kwenye mchezo unaofuata dhidi ya Majimaji utakaochezwa jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingne, Djuma, ameweka wazi kuwa kwake hana shida kuwa msaidizi wa Mfaransa Pierre Lechantre, ambaye ataanza kuiongoza timu hiyo kama kocha mkuu.

Simba tayari imempa mkataba Mfaransa huyo na Djuma, atarejea kwenye nafasi yake ya kocha msaidizi.

“Mimi ni mtu ninayependa kujifunza, naamini nitapata fursa ya kujifunza, kuwa kocha msaidizi itanipa nafasi ya kuendeea kupata mbinu na uwezo kupitia kwa kocha wa juu yangu,” alisema Djuma.

Simba kwa sasa inaongoza ligi kwa tofauti ya pointi mbili dhidi ya Azam FC wanaoshika nafasi ya pili wakiwa na pointi 30, Yanga ambayo nayo inadhaminiwa na SportPesa, inashika nafasi ya tatu baada ya kukusanya pointi 25

    Choose :
  • OR
  • To comment
No comments:
Write comments