Tuesday, January 23, 2018

Kinyesi chaanguka kutoka kwenye ndege

Maafisa nchini India wanashuku kwamba kipande cha kitu chenye barafu kilichoanguka katika kijiji kimoja kaskazini mwa nchi hiyo kilikuwa ni kinyesi kutoka kwa ndege iliyokuwa inapita angani.

Kipande hicho cha uzani wa kilo 10-12 kilianguka katika kijiji cha Fazilpur Badli katika jimbo la Haryana kwa kishindo na kuwashtua wakazi.

Afisa mmoja Vivek Kalia ameambia BBC kwamba baadhi ya wakazi walidhania pengine kilikuwa kitu kutoka anga za juu kilichokuwa kimeanguka.

Uchafu kutoka kwenye vyoo vya ndege huhifadhiwa kwenye matanki maalum.

Mara nyingi uchafu huo hutupwa baada ya ndege kutua.

Lakini maafisa wa kimataifa wa uchukuzi wa ndege wanakiri kwamba wakati mwingine vyoo hivyo huvuja.

Bw Kalia ameiambia BBC kwamba sehemu ya kipande hicho imepelekwa kwenye maabara kwa uchunguzi zaidi, lakini "tunashuku kwamba" ni kinyesi kutoka kwenye ndege.

"Kilikuwa kipande kizito sana ambacho kilianguka kutoka angani Jumamosi asubuhi. Kulisikika kishindo na wakazi walifika mbio kutoka manyumbani mwao kuchunguza ni nini kilikuwa kimetokea," amesema.

"Baadhi ya wakazi walidhani kilikuwa kitu kutoka anga za juu. Wengine walidhani lilikuwa jiwe kutoka anga za juu na nimesikia baadhi walichukua vipande vidogo na kwenda navyo nyumbani," amesema.

Gazeti la Times of India limesema baadhi ya watu walificha vipande mifukoni na kisha kuvihifadhi kwenye majokofu nyumbani.

Afisa mmoja wa utabiri wa hali ya hewa India ambaye alichunguza kipande hicho amesema bila shaka "hakikuwa kimetoka anga za juu."

Desemba 2016, mahakama moja India iliamua kwamba mashirika ya ndege nchini humo yangeadhibiwa iwapo ndege zingeachiliwa kinyesi kutoka angani.

Januari 2016, mwanamke mmoja jimbo la Madhya Pradesh katikati mwa nchi hiyo aliumia vibaya begani baada ya kipande kikubwa cha barafu kutoka angani kuangukia nyumba yake.

Gazeti moja lilisema huenda aligongwa na kipande cha kinyesi kilichokuwa kimeganda.

Kinyesi kutoka kwenye ndege ambacho kimeganda mara nyingi huitwa "barafu ya buluu" kwa sababu ya kemikali ambazo huongezwa kupunguza uvundo na kuyeyusha uchafu huo.

Shirika la uchukuzi wa ndege Uingereza linasema visa vya kaunguka kwa "barafu ya buluu" 25 huripotiwa kila mwaka kutoka kwa safari 2.5 milioni za ndege ambazo hufanywa katika anga ya Uingereza kila mwaka

    Choose :
  • OR
  • To comment
No comments:
Write comments