MWENYEKITI wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Freeman Mbowe, anatarajia kuongoza wabunge 10 katika uzinduzi wa kampeni za uchaguzi mdogo jimbo la Siha, Kilimanjaro.
Katika uzinduzi huo utakaofanyika keshokutwa katika kijiji cha Ngarenairobi, Mbowe na wabunge hao kutoka Kanda ya Kaskazini, kumnadi Elvis Mossi.
Chadema watakuwa wakijaribu kufanya kila liwezekanalo kulirejesha jimbo hilo ambalo lilikuwa mikononi mwao kabla ya Dk. Godwin Mollel kujiuzulu na kujiunga na CCM.
Taarifa iliyopatikana jana na kuthibitishwa na Katibu wa Chadema Mkoa wa Kilimanjaro, Basil Lema, imesema Mbowe ataongozana na wabunge 10 wa Chadema Kanda ya Kaskazini ambao watasambazwa kila kata.
"Tunakuja kimkakati kwa sababu tunataka kufanya siasa ya kisayansi ambayo CCM na vyama vingine hawataamini namna Dk. Mollel atakavyopotea kwenye ramani ya siasa. Tunakwenda kuwaeleza wananchi namna ambavyo amesababisha gharama kubwa za kurudia uchaguzi kwa usaliti,” alisema.
Siku hiyo pia, Prof. Lipumba naye atazindua kampeni hizo kwa kumnadi Tumsifueli Mwanri katika Kijiji cha Ndumeti, West Kilimanjaro.
Wakati Chadema na CUF wakianza mtifuano huo, CCM wao watakuwa wakiendelea kuchanja mbuga katika Kijiji cha Livishi, wakimtumia Naibu Katibu Mkuu (Bara), Rodrick Mpogolo, kumnadi Dk. Godwin Mollel ambaye aliyejiuzulu ubunge na kujiunga na CCM.
Mwenyekiti wa CUF wa Wilaya ya Siha, Faraj Gao, alisema Prof. Lipumba ndiye aliyepangwa kuzindua kampeni hizo na kwamba maandalizi yamekamilika na kinachosubiriwa ni kumalizika kwa kikao cha chama hicho makao makuu.
"Chama cha Wananchi (CUF) ni kweli kimemteua Tumsifueli Mwanri kugombea ubunge wa Jimbo la Siha na sisi tutazindua kampeni zetu Ijumaa," alisema Faraj.
Alipoulizwa Katibu wa CCM mkoa wa Kilimanjaro, Jonathan Mabihya, kuhusu ujio wa Naibu Katibu Mkuu, Mpogolo, alithibitisha kwamba ndiye atakayemnadi Dk. Mollel siku ambayo wapinzani watazindua kampeni zao.
Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Humphey PolePole, akimnadi mgombea huyo, aliwataka wananchi wa Siha kutokufanya tena makosa yaliyofanyika kwa kumchagua mbunge kutoka chama cha upinzani na badala yake sasa wamchague Mollel, ili kushirikiana na chama tawala kutatua kero na changomoto mbalimbali za wananchi wa Siha.
Katika mkutano huo, Polepole aliwaomba wananchi hao wamachague tena katika kipindi hiki, ili akashirikiane na serikali kutatua kero za wakazi wa kijiji hicho na wilaya ya Siha kwa ujumla. Alisema wilaya bado inakabiliwa na changamoto za afya, maji, barabara, ardhi, ajira kwa vijana na upatikanaji wa chakula. Polepole alisema wananchi wa Siha hawana budi kumchagua Dk. Mollel kwa kuwa atakwenda kushirikiana na serikali iliyoko madarakani kutekeleza ilani ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na wakati huu si wa kushindanisha sera tena bali utekelezaji.
Alisema katika uchaguzi mkuu ujao wa 2020 utakuwa mwaka wa kilio na simanzi kwa vyama vya upinzani kwa kuwa CCM imejipanga kuchagua wagombea wenye sifa na uwezo wa kuwatumikia wananchi na si wananchi kuwatumikia viongozi
No comments:
Write comments