Thursday, February 1, 2018

Ridhiwani atoa agizo afisa mtendaji kuondolewa mara moja


Chalinze. Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete ametaka kuondolewa mara moja kwa ofisa mtendaji wa kata ya Vigwaza, Elizabeth Msenga kwa maelezo kuwa ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Ridhiwani ametoa kauli hiyo leo Februari1, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo, kutaka mtendaji huyo kupangiwa eneo jingine la kazi.

Amesema haiwezekani wananchi wanapata matatizo na kukosa mtu wa kuwasikiliza na kuwasilisha kero zao sehemu husika.

“Yaani akija mbunge ndio wananchi wanalalamika jukwaani. Uzembe huu unasababisha wananchi kuwa na hasira na kukichukia CCM wakidhani hakiwasilizi na hakiwajali kumbe ni uzembe wa mtu mmoja tu,” amesema na kuongeza,

"Nimezunguka vijiji zaidi ya vinne kero zinazopewa ni nyingi lakini utatuzi wake upo chini ya Serikali ya kata. Nashangaa hata ofisa mtendaji hayupo katika ziara na si mara ya kwanza, hakuna taarifa ya Serikali iliyoandaliwa.”

Wakati ombi lake la kutaka ofisa huyo kuondolewa likishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo uliokuwa sehemu ya ziara ya mbunge huyo kukagua miradi ya maendeleo, mwenyekiti wa CCM kata ya Vigwaza, Shedeli Mikole amesema hali hiyo inatokana na viongozi kufanya kazi kwa mazoea.

“Ombi lako litafanyiwa kazi kwa sababu Vigwaza kuna tatizo kubwa la utekelezaji wa shughuli za maendeleo,” amesema.

"Mbunge nikuhakikishie hoja hii itafanyiwa kazi na sio siri hapa Vigwaza kuna tatizo la kasi ya utekelezaji shughuli za maendeleo. Huyu mjini hawezi kabisa tumeshamuona siku nyingi anapaswa aende kata nyingine pembezoni mwa mji, "amesema Mikole.

Hata hivyo,  Msenga alipotafutwa kwa njia ya simu na Mwananchi amesema hakuweza kuhudhuria ziara hiyo kwa kuwa ni mgonjwa.

    Choose :
  • OR
  • To comment
No comments:
Write comments