Thursday, February 1, 2018

Yanga yainyooshea mikono Timu ya Ihefu FC


LICHA ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Yanga  kuiondosha Timu ya Ihefu FC kwenye mashindano ya kombe la shirikisho, Kocha msaidizi wa Wanajangwani hao, Shadrack Nsajigwa, amewanyooshea mikono Ihefu kutokana na kiwango walichoonyesha.

Akizungumza baada ya mchezo huo kumalizika katika Uwanja wa Kumbukumbu ya Sokoine jijini Mbeya, Nsajigwa alikiri vijana hao kutoka katika mabonde ya Mpunga wilayani Mbarali kuonyesha mchezo mzuri kuliko Yanga inayodhaminiwa na Kampuni ya Kubashiri Matokeo Michezoni ya SportPesa.

Alisema timu hiyo iliyojaa vijana, ilicheza vizuri na kwa nguvu katika dakika zote 90 na kwamba Yanga wao walianza kuonyesha mchezo mzuri katika dakika 45 za kipindi cha pili.

“Nafurahi tumepata ushindi unaotufanya tusonge mbele katika mashindano haya, lakini vijana wa Ihefu wameonyesha mchezo mzuri kuliko sisi na wamecheza kwa nguvu muda wote, penalti ni bahati na yeyote anaweza kukosa,” alisema Nsajigwa.

Kwa upande wake Kocha Mkuu wa Ihefu FC, Michael Kasegeya, aliwapongeza vijana wake kwa kujituma na kuonyesha kandanda safi na kwamba walifuata maelekezo yake.

Alisema vijana wake walicheza vizuri japo haikuwa bahati yao kusonga mbele kwenye mashindano hayo ambayo Bingwa ataiwakilisha Tanzania katika Kombe la Shirikisho barani Afrika.

Mchezo huo ulianza kwa kasi na kosakosa nyingi ambapo katika dakika ya pili ya Mchezo mchezaji wa Kimataifa wa Yanga kutoka nchini Burundi alikosa bao baada ya shuti lake la mguu wa kushoto akiwa ndani ya 18 kupaa juu ya lango.

Timu ya Ihefu FC, ilipata bao la kuongoza katika dakika ya 35 kipindi cha kwanza kufuatia Mlinzi wa Yanga, Andrew Vincent ‘Chikupe’ kujifunga katika harakati za kuokoa mpira uliokuwa unazagaazagaa langoni kwao.

Bao hilo lilidumu mpaka dakika 90 zikamalizika, lakini katika dakika sita za majeruhi Ihefu wakijiaminisha ushindi, dakika ya (90+3) mchezaji Obrey Chirwa wa Yanga aliangushwa na walinzi wa Ihefu FC na mwamuzi wa mchezo huo akaamuru upigwe mkwaju wa penalt, ambayo ilizamishwa kimyani na Chirwa mwenyewe.

Mchezo huo ulimalizika kwa timu hizo kufungana bao 1-1.  Yanga waliibuka na ushindi 4-3 kwa mikwaju ya penalti.

    Choose :
  • OR
  • To comment
No comments:
Write comments