Thursday, February 1, 2018

Rais Magufuli atangaza Kiama kwa wanaochelewesha kesi Mahakamani


Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametangaza 'kiama' kwa watumishi wa umma ambao wamekuwa wakichelewesha kesi mahakamani hususan wanasheria huku akisisitiza mwezi huu hautaisha atawashughulikia wote kwani anawafahamu.

Pia, Rais Magufuli ametoa mwezi huu kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kukamilisha kanuni za msaada wa kisheria.

Akizungumza leo Februari mosi, 2018 katika siku ya Sheria, Rais Magufuli amesema usimamizi wa sheria na utoaji wa haki bado una changamoto, wapo wachache uadilifu wao na matendo yao yanachafua vyombo vyeti.

"Wanatoa hukumu zinazopendelea watu, kuchelewesha hukumu au kesi na kati ya 112 waliofukizwa au kustaafishwa 27 walikuwa Mahakimu na wote walipokwenda Mahakamani walishinda," amesema Rais Magufuli na kuongeza,

"Walikuwa Mahakimu 14 walifukuzwa kazi, 67 watumishi wa kawaida walifukuzwa kazi. Wito wangu kwa vyombo vingine IGP, Mkuu wa Magereza, Takukuru muige mfano wa Profesa Juma (Ibrahim Juma-Jaji Mkuu,"
"Majaji mnisamehe. Sitalalamika tena, nishajifunza, najua wapi tunakosea, mwaka jana nililalamika, mwaka huu sitalalamika, najua jinsi ya kufanya na wala mwezi huu hautaisha," amesema Rais Magufuli

Pia, Rais Magufuli amemwagiza Jaji Mkuu, Profesa Juma kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama kufanya uchunguzi kwa baadhi ya majaji ambao wao kila likizo zao wanakwenda mapumziko ulaya jambo linalotia minong'ono ya nani anawagharamikia wakati mishahara yao inajulikana.

Rais Magufuli amewanyooshea vidole Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Naibu Mwanasheria Mkuu, Gerson Mdeme wameshindwa kuandaa kanuni za msaada wa kisheria.

"Bunge limepitisha, mimi nimesaini lakini Waziri wa Katiba na Sheria tena Profesa, AG, Naibu AG wote wapo, wanakula mishahara, magari ya kiyoyozi wanayo lakini miezi tisa wameshindwa kuandaa kanuni," amesema Rais Magufuli

"Wakati mwingine na mimi najitathimini nawachaguaje chaguaje hawa. Nataka mwezi huu kanuni ziwe zimekamilika kwani wakati mwingine majaji na Mahakama wanalalamikiwa bure," ameongeza

Rais Magufuli amesema vitendo vya rushwa vipo na "nina taarifa nyingi kweli kweli, rushwa haifichiki na Jaji Mkuu hao majaji wanaokwenda ulaya kufuatilia vibali vyao."

Awali akimkaribisha Rais Magufuli, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria kupitishwa kwa Kanuni ili kuruhusu kuanza kutumika kwa Mahakama inayotembelea ili kusogeza huduma  za kisheria karibuni zaidi.

Amesema umuhimu wa Mahakama lazima upewe kipaumbele na kwa kutumia wiki ya Sheria watafakari walipotoka, walipo na wanapokwenda.

Amesema Mahakama imejiwekea malengo ya kuongeza kasi, uwazi na uadilifu na hawataki kusikia shauri lake lipo wapi na kwa jani yupi au kusikia jalada lake limepotea yote hayo yanaondolewa na mfumo wa Tehama.

"Wananchi wa Tanzania, watarajie huduma bora za uendeshaji wa kesi, uwazi na huona hukumu kwani Tehama itarahisisha yote haya na sisi majaji, mahakimu na watendaji wa Mahakama tubadili fikiri zetu na kuijua Tehama kwani karne hii inahitaji kwenda na wakati," amesema Profesa Juma

Amesema utaratibu unafanyika ili kukamilisha mfumo wa menejimenti za kesi ambayo itatumika kulipa ada, uendeshaji wa kesi kwa masafa ya mbali.

Amesema idadi ya majaji waliopo hayaendani na majalada wanayopewa kuyasikiliza kwani majaji waliopo ni 62 pekee na kila mwaka wanabeba majalada 535 badala ya 225 wanayopaswa kuyasikiliza.

"Huu ni mzigo mkubwa sana na iko nje ya makubaliano kwamba kila jaji amalize majalada 225 lakini kwa idadi hii ni mzigo mkubwa sana," amesema Profesa Juma

Amesema mpaka sasa ni mikoa 14 kati 26 pekee ndizo zenye Mahakama Kuu ambapo alidokeza malengo ni kuwa na Mahakama Kuu katika mikoa 22 ifikapo mwaka 2020.

Jaji Mkuu amesema malengo yao ifikapo mwaka 2020 wilaya zote 139 za Tanzania bara zinakuwa na Mahakama za wilaya.

Amesema katika kipindi cha 2016/17, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilisikiliza malalamiko ya kimaadili 143 ambapo kati ya waliofukuzwa au kustaafishwa ni 112 na 17 walirudishwa kazini.

"Hatutamwonea mtumishi lakini hatutamvumilia mtu anayetupaka matope sisi kama Mahakama," amesema Jaji Mkuu

Kwa upande wake, Makamu wa rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi amesema ukiweka pembeni tofauti za kiitikadi, kiongozi anayetuunganisha ni Rais Magufuli.

"Matarajio yake (Rais Magufuli) hayafiki kwetu sisi na kwa maoni yangu matarajio ya kiongozi wangu huyu yanaakisi matarajio ya wananchi," amesema Ngwilimi

Akitoa wito kwa Majaji, Ngwilimi amesema "Mahakama inafaa kuwa mahali iliyotukuka kwani ni mahali pekee tunapokuwa na migogoro, pale tunapoililia sheria tunakwenda mahamakani na hii haijalishi aina ya mtu."

"Tusiitumie Mahakama kama majaribio, maabara au jumba la kamari. Majaji msiitumie hata Mara moja kwani mnalindwa kisheria na msimamie hilo ili Mahakama isionekane ya ajabu ajabu," ameongeza

Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gerson Mdeme amesema utoaji haki unahitaji ushirikiano kutoka wa wadau mbalimbali na ofisi ya Mwanasheria Mkuu imekuwa ikifanya hivyo kwa maslahi ya Taifa na wananchi.

Mdeme alitolea mfano kati ya Julai na Desemba mwaka jana iliendesha mashtaka mbalimbali ya jinai yenye thamani ya Sh45 bilioni na dola za Marekani milioni tisa ambazo kama tusingefanya hivyo Serikali ingetakiwa kulipa kiasi hiki cha fedha.

"Kwa utumiaji wa tehama utaongeza utoaji haki kwa haraka na vyombo vingine kama baraza la kata, biashara, mahakama na mengine yanahitaji kuitumia ili kumaliza kesi haraka na kwa wakati

," amesema Mdeme

Amesema ni muhimu kuwa na bajeti na rasilimali watu zinazojitosheleza ili kuhimili matumizi ya Tehama ambayo inaleta mapinduzi makubwa ya utoaji haki.

"Kupungua kwa gharama, kupunguza urasimu, kuwahisha utoaji wa haki na watumishi wasio waaminifu mfumo huu wa Tehama utawaumbua kwani shughuli zitafanyika kwa uwazi," amesema Mdeme

"Tumejiandaaje na wizi wa mitandao, watu wetu wameandaliwa kiasi gani katika matumizi ya Tehama, tumejiandaaje kuweka mazingira salama kwa maslahi ya Watanzania," ameongeza

Siku hiyo ya sheria yenye kauli mbiu 'Matumizi ya Tehama katika utoaji haki na kwa wakati' ilitanguliwa na maombi yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa dini walioombea Serikali, Mahakama na Bunge.

Amesema angefurahi  kuona IGP naye anatoa majina ya polisi wanaochelewesha upelelezi hata kama mtu kashikwa na dawa za kulevya au mkuu wa magereza watu wanaoingiza simu gerezani.

    Choose :
  • OR
  • To comment
No comments:
Write comments