Thursday, February 1, 2018

Mbunge CUF afunguka Wabunge kutelekeza watoto wao

 Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji leo Februari 1, 2018 ameibua tuhuma bungeni, akidai baadhi ya wabunge wenzake wamewatelekeza watoto wao.

Amesema katika mkutano wa Bunge uliopita,  mmoja wa mtoto aliyetelekezwa na wawakilishi hao wa wananchi, aliletwa bungeni na mama yake.

Akizungumza katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, Khatibu amesema sasa chanzo cha watoto wa mitaani kimethibitika kwa sababu wanaume wengi wanashindwa kutunza familia zao.

“Mheshimiwa mwenyekiti Bunge lililopita nilishuhudia wanawake wengi wakija na watoto wao pale nje (ya viwanja vya Bunge) wakidai kutelekezwa na wazazi wenzao ambao ni wabunge wanaume. Tabia  hii itakwisha lini na wabunge waanze kutunza watoto wao," amesema Khatibu.

Khatibu ameungwa mkono na mbunge wa Kavuu (CCM), Dk Pudensiana Kikwembe, aliyetaka jambo hilo kuwekwa wazi ili kujua kama wabunge hao wamezaa na wabunge wenzao au wamezaa na watu wengine lengo likiwa ni kujua jinsi ya kuwasaidia.

Katika ufafanuzi wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema kitendo cha kutelekeza watoto ni kinyume na sheria za nchi, kuwataka wananchi, hasa wanaume kuacha tabia hizo.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema Bunge halina taarifa za wabunge kutelekeza watoto..

Kuhusu hoja kama wamezaa na wabunge wenzao ama la, Dk Ndugulile ameomba kiti cha Spika kufuatilia suala hilo kwa maelezo kuwa yeye hawezi kulijibu

    Choose :
  • OR
  • To comment
No comments:
Write comments