Uzinduzi wa hati ya Kielektroniki yaibua mambo 10
Dar es Salaam. Unaweza kusema uzinduzi wa hati ya kielektroniki ya kusafiria uliofanywa jana na Rais John Magufuli umeibua mambo 10.
Baadhi ya mambo hayo yalizungumzwa na kiongozi huyo mkuu wa nchi katika hotuba yake wakati wa uzinduzi huo jijini Dar es Salaam, mengine kuelezewa na Kamishna Jenerali wa Uhamiaji, Dk Anna Makakala na Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida).
Ukiacha ulazima wa Mtanzania kuwa na Kitambulisho cha Taifa na Sh150,000 ili kupata hati hiyo mpya, kuna mambo mengine matano yaliibuka baada ya uzinduzi huo.
Mambo hayo ni sifa za hati hiyo zikiwamo za kuwa na alama nyingi za usalama, kuweza kuhifadhiwa katika programu ya simu ya mkononi “App”, hati za kusafiria za zamani kutumika hadi mwaka 2020, ikiwa mtu ana safari ya dharura na hana Kitambulisho cha Taifa, atapewa hati ya dharura na kuitumia si zaidi ya miaka miwili.
Mengine ni kutokuwapo uwezekano wa kughushi hati mpya, utaratibu wa Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa (Nida) kutoa vitambulisho, hati mpya kuwa na kurasa nyingi kuliko ya zamani na hivyo kuweza kutumika muda mrefu zaidi na Mtanzania kupata huduma ya haraka katika balozi ikiwa ataipoteza.
Akitoa maelezo kabla ya uzinduzi huo uliofanyika Makao Makuu ya Uhamiaji Kurasini, Dk Makalala alisema mfumo wa uhamiaji mtandao ni muunganiko wa mifumo mbalimbali ambayo imesanifiwa kufanya kazi kwa pamoja, kutoa taarifa kwa watumiaji na wadau wa huduma za kiuhamiaji.
Alisema kupitia mfumo huo, Idara ya Uhamiaji imeanza kutoa hati za kusafiria, viza za kielektroniki, vibali vya ukaazi vya kielektroniki na udhibiti wa mipaka wa kielektroniki.
Alisema hati mpya ni ya kisasa ikiwa na alama nyingi zaidi za usalama, ni ngumu kughushi, “Ina kurasa nyingi zaidi ukilinganisha na ya zamani hivyo kumwezesha mtumiaji kuitumia zaidi na kwa muda mrefu.
“Pasipoti hii inamwezesha mtumiaji kuwa na nakala ya pasipoti ya kielektroniki kwenye simu yake ya kiganjani baada ya kupakua ‘app’ ya hati yake ya kusafiria katika simu.”
Alisema Mtanzania anapokuwa na nakala ya hati yake katika simu, itamuwezesha kupata huduma ya haraka katika Balozi za Tanzania nje ya nchi, ikiwa aitapoteza.
Kuhusu utaratibu wa kuipata, Dk Makakala alisema sharti kuu ni lazima mhusika awe na Kitambulisho cha Taifa.
“Nitoe wito kwa wanaoataka kuja kuomba pasipoti mpya waje na kitambulisho cha Taifa ndio sharti muhimu. Pasipoti za kawaida zinazotumika sasa zitaendelea kutumika hadi Januari 2020 kisha zitaondolewa kabisa,” alisema.
Alisema hati za kusafiria za Afrika Mashariki zilizokuwa zikitumika awali, hazitatolewa tena baada ya kuanza kutolewa hati za kusafiria za kimataifa.
Alipotakiwa na Mwananchi kutoa ufafanuzi kuhusu hati hizo mpya, Dk Makakala alisema “Tunaendelea kutoa hati za zamani katika kipindi cha miaka miwili hadi Januari 2020 tutakapositisha. Hatuwezi kusitisha moja kwa moja, tupo katika kipindi cha mpito.”
Alisema ikiwa mtu ana hati ya kusafiria ya zamani na anataka kubadili apate mpya, atalazimika kuambatanisha maombi yake na kitambulisho cha Taifa.
“Tunafanya hivyo kwa sababu kuna taarifa tunahitaji kuzichukua ingawa mhusika tayari tutakuwa na ukaribu naye kwamba tayari si mgeni kwetu,” alisisitiza.
Awali, alisema mradi huo ulianza mwaka 2013 na Septemba 2017 walisaini mkataba na kampuni ya HDI ya Marekani na kwamba hadi kufikia Desemba mwaka huu, mfumo mzima utakuwa umekamilika ikiwa ni pamoja na kuufunga katika balozi za Tanzania zilizo nje ya nchi.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Mwigulu Nchemba alisema gharama ya kupata hati mpya ni Sh150,000 na mhusika ataitumia kwa kipindi cha miaka 10.
Alipoulizwa kuhusu idadi ya Watanzania waliopata Vitambulisho vya Taifa, msemaji wa Nida, Rose Mdami alisema wengi wamepata.
“Kwa asilimia kubwa Watanzania wengi wamepata vitambulisho na tunaendelea kutoa katika mikoa 20. Lengo letu ikifika Desemba mwaka huu Watanzania wenye sifa wawe wamepata.”
Katika hotuba yake ya uzinduzi, Rais Magufuli alitoa sababu za kumteua Dk Makakala, Februari 10 mwaka jana, kwamba ni kutokana na matatizo mengi yaliyokuwamo Uhamiaji.
Alisema miaka ya nyuma, Uhamiaji iligubikwa na matatizo mbalimbali ikiwamo utoaji ovyo wa vibali vya uraia hata kwa watu ambao hawakuwa na sifa za kupata uraia.
“Kuna raia wengi walipata uraia bila sifa na wapo waliopata uraia na vyeo vya juu kabisa serikalini. Hii ndiyo sababu niliamua kumteua mwanamama kuongoza idara hii muhimu na wanawake ni waaminifu sana, ameanza kutatua matatizo haya,” alisema Rais Magufuli.
Rais Magufuli alimwagiza kamishna huyo kuwachukulia hatua kali, ikiwamo kuwavua vyeo watumishi wa Uhamiaji ambao watashindwa kutekeleza wajibu wao ipasavyo, ikiwa ni pamoja na kudhibiti wahamiaji haramu.
“Haiwezekani wahamiaji haramu wanakamatwa Mbeya halafu wamepita Kilimanjaro, Manyara, wamepitaje kote huko hadi wakafika Mbeya? Au wamepita Chato (Geita), Buboka (Kagera) hadi Singida, huko walikopita hakuna watu?” alihoji.
Kuhusu mchakato wa mfumo huo wa utoaji hati mpya, Rais Magufuli alisema umegharimu Sh127.2 bilioni ikilinganishwa na makadirio yaliyowekwa awali ya Sh400 bilioni.
“Hapa tumeokoa fedha nyingi za Watanzania, kuna watu walikuwa wamejiandaa kutupiga na kuchukua hizo Sh400 bilioni, lakini tukatumia vyombo vyetu mbalimbali, tukafanya uchunguzi na tumefanikiwa kutekeleza mradi huu kwa gharama nafuu,” alisema.
Uzinduzi huo ulihudhuriwa na mke wa Rais Mama Janeth Magufuli, Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk Ali Mohamed Shein, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa Majaliwa.
Wengine ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahim Hamis Juma, Jaji Mkuu wa Zanzibar, Omar Othman Makungu, Spika wa Baraza la Wawakilishi, Zubeir Ali Maulid, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Tulia Ackson, Rais mstaafu wa Awamu ya Pili, Ali Hassan Mwinyi na Rais mstaafu wa Zanzibar, Amani Abeid Karume.
No comments:
Write comments