Tuesday, February 20, 2018


Watu 250 wauawa Ghouta wakiwemo watoto

Idadi ya watu waliokufa katika mashambulizi ya anga yanayotekelezwa na vikosi vya serikali huko huko Ghouta mashariki imefikia 250 ambapo kati ya idadi hiyo 50 wakiwa ni watoto.

Umoja wa mataifa nchini Syria umesema una mashaka makubwa juu maisha ya mamia ya raia ambao bado wapo katika eneo linalolengwa na mashambulizi ya anga ya vikosi vya serikali ya Syria katika eneo la Ghouta mashariki.

Mashambulizi hayo yaliyoanza siku ya jumapili bado yanaendelea na kusababisha vifo na majeruhi wengi wakiwemo watoto.

Umoja wa mataifa umeelezea mashaka yake juu ya kutokea Allepo nyingine,ambapo ukombozi wa mji huo mwaka 2016 pia ulisababisha vifo vya mamia ya raia kufuatia mashambulizi ya vikosi vya serikali.

Geert Cappelaere afisa kutoka UNICEF ameimabia BBC kuwa watoto ni miongoni mwa waliouawa

''Makundi ya watoto ni miongoni mwa watu wanauawa huko Ghouta Mashariki.watoto hawa wanalipa gharama ya uhai wao kwa jambao ambalo hawahusiki.Kama tunahitaji kuzuia umwagikaji wa damu Zaidi kwa watoto ni lazima tukubali kupata majeraha pia,na pia safari hii tunapata somo0 juu ya namna tunavyo takiwa kuwalinda watoto na kuona kwamba ni wajibu kila mmoja kuwalinda watoto.''

Idadi ya watu waliokufa ndani ya siku mbili ya mashambulizi hayo imepanda na kufikia 250 kwa mjibu wa ripoti kutoka Ghouta mashariki karibu na mji mkuu Damascus,huku kati yao 50 wakiwa ni watoto.

Okwi amvuruga Chirwa Yanga

Chirwa.

MSHAMBULIAJI wa Simba, Emmanuel Okwi, ameonekana kumuumiza kichwa straika wa Yanga, Obrey Chirwa ambapo imebainika kuwa ndiye chanzo cha Mzambia huyo kushindwa kuungana na wenzake kwenye safari ya kuelekea Shelisheli kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya St Louis.

Chanzo makini kutoka ndani ya Yanga kimeli­ambia Championi Jumatano kuwa Okwi ndiye aliyechangia Chirwa ashindwe kwenda Shel­isheli baada ya kulazimisha kucheza mchezo wao wa ligi kuu uliopita dhidi ya Majimaji huku akiwa na majeraha ambapo alipanga kuongeza idadi ya mabao ili kumpita Mganda huyo.


Okwi.
“Ukweli ni kwamba Okwi ndiye ambaye amechangia Chirwa kubakia hapa Dar baada ya kushindwa kwenda Shelisheli kama wen­zake ambavyo walifanya kwa sababu Chirwa alilazimisha kucheza ile mechi na Majimaji huku akiwa anaumwa.
“Yeye alipanga atumie mchezo ule kama sehemu ya kumzidi Okwi mabao sasa bahati mbaya ni kwamba baada ya mchezo kumal­izika lile jeraha likazidi kuwa kubwa hivyo kusababisha hadi jina lake litolewe katika wale ambao wanasafiri kuelekea nchini humo kwa ajili ya mchezo wetu.
“Hata hivyo, sasa hivi bado anatamani kupo­na haraka kwa kuwa anataka kurudi uwanjani mapema ili afunge na awe mfungaji bora wa ligi,” kilisema chanzo hicho. 

Pam D ajikita kwenye Singeli


MSANII wa Bongo Fleva, Pamela Daffa ‘Pam D’ ameamua kugeukia muziki wa singeli na kuahidi kuliteka soko hilo, kwa kuwa anaamini muziki huo bado haujapata mwanamke anayeumudu.

Akipiga stori na Risasi Vibes, Pam D alisema yupo kwenye maandalizi ya mwisho ya kuachia wimbo wake wa singeli ambao amemshirikisha Msaga Sumu hivyo amejipanga vilivyo kuleta mapinduzi ya hali ya juu kwenye muziki huo.

 “Nimeamua kuimba Singeli kutokana na ushawishi mkubwa nilioupata kwa Msaga Sumu maana ni mtu wangu wa karibu ambaye tunashauriana mengi, si kwamba nitaacha Bongo Fleva ila tu nataka kuwaonyesha mashabiki wangu kwamba muziki wa aina yoyote naweza kufanya na nikatusua,” alisema

Serikali yahakiki bajeti mil. 80/- mazishi Akwilina


FAMILIA ya Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Maftah (22), ambaye alifariki kwa kupigwa risasi na polisi Ijumaa iliyopita, imeandaa bajeti ya Sh. milioni 80 ya mazishi yake, lakini serikalini imesema itakaa na ndugu hao kujiridhisha.

Akwilina alifariki baada ya kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni na polisi waliokuwa wakijaribu kutawanya maandamanao ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Ijumaa jioni.

Baada ya kifo hicho, serikali iliahidi kugharamia mazishi na juzi kikao cha msiba huo, pamoja na mambo mengine, kiliandaa bajeti ya Sh. milioni 80 ambayo ilikabidhiwa serikalini jana.

Msemaji wa familia hiyo, Festo Kavishe, aliliambia Nipashe kuwa baada ya kuikabidhi, walitaraji kukutana na wawakilishi wa serikali kwa ajili ya kuichanganua.

Lakini akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema wamepokea mapendekezo hayo na kwamba walitarajia kukaa na familia "jioni" kwa ajili ya kuipitia, ili kujua uhalisia wake.

"Ni kweli wametupa mapendekezo yetu, lakini serikali ina utaratibu wake," alisema Prof. Ndaliachako. "Katibu Mkuu wangu ameyapokea mapendekezo hayo na watakaa jioni ili kupitia kipengele kwa kipengele."

Alisema serikali iliipa uhuru familia hiyo kufanya maandalizi na kuandaa mapendekezo, ikiwamo bajeti ya mazishi hayo, kwasababu iliona si busara kuwaingilia.

"Tutakaa kuiangalia ili kujiridhisha na uhalisia wa mapendekezo yao kwa sababu serikali ina utaratibu wake."

Awali Kavishe alisema bajeti waliyoiandaa inaonyesha jeneza la marehemu litanunuliwa kwa Sh. milioni 1.5, malipo ya hospitali Sh. 200,000, gari la kubeba mwili Sh. milioni tatu, magari ya msafara makubwa matano kwa jumla ya Sh. milioni 20 na chakula cha njiani kwa wasafiri Sh. milioni tatu.

Aidha, bajeti hiyo inaonyesha bajeti ya chakula kwa siku tatu msibani Mbezi mkoa wa Dar es Salaam kuanzia asubuhi hadi jioni ni Sh. milioni 10.

"Mahitaji mengine ni viti 200 kwa gharama ya Sh. 400,000, turubai tatu kwa gharama ya Sh. 600,000, fedha ya muziki na kumlipa mshereheshaji Sh. 400,000 picha za kumbukumbu Sh. milioni moja na maji ya kunywa Sh. 50,000," alisema.

Kavishe alisema kamati imeandaa bajeti nyingine ya siku tano ambayo itatumika kwenye shughuli ya mazishi Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo gharama ya chakula kwa siku zote ni Sh. milioni 30.

Alisema muziki na mshereheshaji kwa siku zote tano ni Sh. milioni mbili, maturubai manne kwa gharama ya Sh. milioni moja, viti 400,000 na kaburi la kisasa Sh. milioni tatu.

"Maua na mataji tumeweka Sh. milioni moja, mapambo Sh. 500,000 na dharura Sh. milioni mbili," alisema zaidi Kavishe na kwamba "kwa ujumla bajeti nzima ya shughuli hii kwa siku nane itakuwa ni Sh. milioni 80."

HATUA ZA KISHERIARais John Magufuli alisema katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Twitter Jumapili "Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili."Rais Magufuli pia alielezea kusikitishwa "sana" na kifo cha Akwilina, na kutoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huo.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam siku hiyo pia, Waziri Ndalichako alisema Akwilina alikuwa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi na Ugavi katika chuo hicho.

"Wizara yangu itagharamia mazishi yake hadi hapo atakapopumzishwa katika makao yake ya milele," alisema Prof. Ndalichako. "Tutasimamia shughuli zote za msiba huo.

"Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki... kwa uongozi wa NIT, kwa wanafunzi na wananchi wote."Serikali imepata pigo kubwa kwa sababu inawekeza pesa nyingi katika kuwasomesha wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu kwa kuwapa mikopo."

Aidha, Prof. Ndalichako alisema siku ya Ijumaa Akwilina alikuwa njiani kupeleka barua ya kuomba kufanya kazi kwa vitendo katika moja ya kampuni zilizopo Bagamoyo mkoa wa Pwani.

Marehemu alipanda daladala linalofanya safari kati ya Mabibo na Makumbusho katika kituo cha NIT na kufuatia maelezo ya waziri kwamba alikuwa akielekea Bagamoyo, ilikuwa ashuke mwisho wa safari kabla ya kuunganisha daladala nyingine kwenda Bunju Sokoni au Tegeta Nyuki zilizo stendi za Bagamoyo.

Taarifa za kipolisi zilizotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita zilisema mwili wa marehemu aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma katika daladala hiyo yenye namba T558 CSX aina ya Nissan Civilian, ulikutwa ukiwa na jeraha kubwa kichwani lililoonekana kutokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali, kilichoingia upande wa kulia na kutoka upande wa kushoto.


Mkulima anaswa akiuza Bangi


Polisi walivyomnasa mkulima akiuza bangi
Polisi mkoani Manyara inamshikilia mkulima na mkazi wa Galapo, Emmy Nombo (62), kwa madai ya kujihusisha na biashara ya bangi.

Kamanda wa Polisi wa mkoa, Augustino Senga, alisema tukio hilo lilitokea Alhamisi, majira ya 7:45 mchana katika Kijiji cha Mwada, wilayani Babati.

Alikamatwa akiwa na misoko 858 ya bangi sawa na kilo mbili na nusu.

“Askari wetu wakiwa doria walimtilia shaka mama huyo, askari wa kike wakamkagua na kumkuta ana bangi ambayo alikuwa ameifungia kwenye maungo yake,” alisema.

Alisema mtuhumiwa huyo alikuwa akisafiri kutoka Arusha kwenda Babati akiwa kwenye gari aina ya Toyota Noah.

“Ukimwaangalia huwezi kuamini kuwa anafanya biashara hii, hata hivyo, sisi hatuangalii umri, unadhifu wa mtu, cheo cha mtu, rangi, dini wala kabila kwa kuwa uhalifu hauangalii vitu hivyo,” alisema.

Alisema mtuhumiwa anaendelea kuhojiwa ili kupata taarifa zaidi  zitakazosaidia polisi katika uchunguzi wake ikiwa ni pamoja na kuwabaini watu anaoshirikiana nao.

Kamanda Senga, alisema askari wake wamejipanga kikamilifu kuhakikisha wanapambana na wahalifu ambao watataka kuutumia mkoa huo kuwa ni  kichochoro cha kufanyia uhalifu au kupitisha bidhaa haramu.

Gari Jipya Analotembelea Samatta Ubelgiji hili hapa

 Moja kati ya majina makubwa katika soka kutokea ukanda wa Afrika Mashariki basi huwezi kuacha kutaja jina la nadhoa wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars anayecheza soka la kulipwa katika club ya KRC Genk ya Ubelgiji Mbwana Samatta.

Samatta ni moja kati ya mastaa wa soka ambao hawapendi kuweka mali zao hadharani mara kwa mara lakini leo amepost picha ya gari nyeupe lakini kwa mujibu wa maneno yake aliyoyaandika May 26 2015 katika picha ya Range Rover yake aliyoipost instagram, gari ya leo pia inatajwa kuwa ni lake.

“Hello insta friends off to trainning this morning #Vboss hii picha inamaelezo mengi sana ambayo nahisi nikiyaandika apa naweza kuharibu pia, bora nikae kimya lkn nadhan picha yenyewe itatoa somo especially kwa wachezaji uzao wa sasa ktk soka la tanzania.
NB.nshaacha toka 2012 kupiga picha kwny magar ya watu.”

Hivyo baada ya leo kupost picha Mbwana Samatta akiwa katika gari nyeupe, wengi wameatafsiri tu hiyo ni gari yake mpya japokuwa kwenye caption ameweka emoj pekee lakini kwa mujibu wa maneno yake kuwa “Nishaacha toka 2012 kupiga picha kwny magar ya watu” aliyoiandika mwaka 2015 inadhihirisha kuwa gari hilo ni lake, hii ni gari ya tatu Mbwana Samatta kwa gari zake zilizopo Ubelgiji baada ya Mercedes Benz mbili nyekundu na nyeusi alizowahi kuzipost

Hii ndio rekodi aloiweka Messi


NYOTA wa Klabu ya Barcelona na Timu ya Taifa ya Argentina, Lionel Messi, amevunja rekodi ya kutofunga goli lolote dhidi ya Chelsea ya Uingereza pindi timu hizo zinapokutana.

Imemchukua mchezaji kutumia dakika 730 na mechi 9 kufunga bao lake la kwanza katika michuano ya Klabu Bingwa Barani Ulaya (UEFA), ikiwa ni dakika ya 75 ya mchezo usiku wa kuamkia leo.

Messi ambaye amekuwa yuko katika kikosi kimoja na Andres Iniesta tangu aanze kuichezea Barcelona, alikuwa hajawahi kuzitikisa nyavu za Chelsea hata mara moja.

Iniesta ndiye alimsaidia Messi kufunga bao hilo kwa pasi safi ikitokea upande wa kushoto mwa uwanja wa Stamford Bridge na kuizamisha nyavuni fasta.

Bao lake la kusawazisha limekuwa muhimu kwa Barcelona ambayo imekuwa na faida ya goli moja la ugenini, kabla timu hizo hazijakutana tena katika mchezo wa marudiano utakaopigwa Camp Nou, Jumatano ya Machi 14, 2018

Dayna atundikwa mimba

MREMBO anayekimbiza kwenye Bongo Fleva, Mwanaisha Said ‘Dayna Nyange’ amejazwa kitumbo ndii kinachodaiwa kumpeleka puta na ndiyo sababu ya kuwa kimya kwenye muziki.
Habari ilizozipata Za Motomoto News ni kwamba mwanamama huyo ana ujauzito mkubwa ambao umekuwa ukimsumbua na mara nyingi amekuwa akijificha kwa kuwa hataki watu wengi wajue kama yupo katika hali hiyo.
“Si unajua Dayna alipata mpenzi Mzungu? Nadhani ndiye ameamua kumzalia na hataki kabisa kumtaja baba kijacho wake kwani hata marafiki zake wa karibu ametuficha,” alisema rafiki wa Dayna ambaye aliomba hifadhi ya jina lake.
Hivi karibuni Dayna, kwenye ukurasa wake wa Mtandao wa Kijamii wa Instagram aliweka picha yake ikimuonesha ujauzito wake ukiwa mkubwa na mashabiki wake kuanza kumpongeza kwa hatua hiyo.
Za Motomoto News ilimtafuta Dayna na kumuuliza kuhusu ujauzito wake pamoja na tetesi za kwamba anazaa na Mzungu ambapo alijibu kwa kifupi:
“Sitaki kuzungumzia mambo ya ujauzito wangu na baba kijacho maana ni maisha yangu binafsi.”

Thursday, February 1, 2018

Mtanzania ahukumiwa kunyongwa Uganda
Mahakama Kuu nchini Uganda imemuhukumu raia mmoja wa Tanzania kunyongwa hadi kufa baada ya kupatikana na hatia ya mauaji.

Mtanzania huyo aliyetambulika kwa jina la Matule Chresporeto Coleheri mkazi wa Bukoba anadaiwa kumuua mfanyakazi mwenzake katika shamba moja lililoko eneo la Wakyuto wilayani Nakaseke.

Akisoma hukumu hiyo, Jaji Steven Mubiru amesema baada ya kusikiliza ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka, mahakama imejiridhisha kuwa Matule ndiye alitenda kosa hilo.

Amesema  mashahidi watatu walioshuhudia tukio hilo wameiridhisha mahakama kuwa Thomas Kamuhebwa aliuawa na mtuhumiwa huyo. Mwili wa Kamuhebwa ulikutwa ukiwa umetupwa katika shimo moja na kufungwa katika begi. Mwili uliokotwa  karibu na makazi ya mshtakiwa.

Hata hivyo, mbele ya mahakama hiyo Matule alijitetea kutohusika katika mauaji hayo na kudai tuhuma hizo zilitengenezwa na watu waliotaka kuiba magogo yake aliyoyaandaa kwa ajili ya kuzalisha mkaa.

Awali, ilielezwa mahakamani hao kuwa Matule ni mhamiaji kutoka Tanzania aliyekuwa akifanya kazi za vibarua na kwamba Februari 6, 2014 alimuua Kamuhebwa kwa sababu zisizo julikana na kufukia mwili wake katika shimo.

Kifo cha Msanii Radio chamgusa Rais Museven
Kufuatia kifo cha msanii wa muziki Radio aliyefariki alfajiri ya leo nchini humo, Rais wa Uganda Yoweri Museven ameonyesha hisia zake kwa kuguswa na kifo cha msanii huyo.

Kupitia  mtandao wa kijamii wa Twitter, Rais Museven ameandika “Have been told about the untimely death of musician Moses Ssekibogo aka Mowzey Radio. I had only recently made a financial contribution towards his treatment and hoped he would get better. He was a talented young person with a great future ahead of him. May he rest in peace.”

Taarifa za kifo cha msanii huyo zinakuja baada ya  siku chache zilizopita Rais Museven kutoa kiasi cha  Milioni 30 kwa ajili ya  matibabu ya msanii huyo.

Vile vile wasanii mbalimbali kama Navio, Diamond, Eddy Kenzo, Professa Jay  na wengineo wametumia kurasa zao   za mitandao yao ya kijamii kama Instagram na Twitter kutoa pole kwa familia yake.

Baada ya kutangazwa taarifa za kifo mashabiki wa msanii huyo na wa Goodkife walifika hospitali hapo kushuhudia kinachoendelea.
Msigwa afunguka haya Bungeni
Kamatakamata ya viongozi wa vyama vya siasa, wakiwemo wabunge leo Februari1, 2018 imemuibua bungeni Mbunge wa Iringa Mjini (Chadema), Mchungaji Peter Msigwa kusema vitendo hivyo ni ukiukwaji wa haki za binadamu.

Msigwa ameibua hoja hiyo katika kipindi cha maswali na majibu, baada ya kuulizwa swali la nyongeza akihoji sababu za wanaokamatwa kushikiliwa kwa muda mrefu katika vituo vya polisi.

“Mimi ni mhanga wa jambo hili napenda kujua msingi wake ni nini, lini mambo haya yatakoma,” amesema.

Mbunge huyo amehoji lini taarifa ya Tume ya Haki za Binadamu ambayo ilieleza kuhusu kamatakamata itawasilishwa bungeni kwa ajili ya kujadiliwa.

Akijibu suala hilo, Naibu Waziri Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Kazi, Ajira na Walemavu Anthony Mavunde amesema “..,  naomba wananchi wawe watulivu na kujiepusha kufanya mambo yasiyofaa.”

Amesema kwa mujibu wa Katiba, tume hiyo inapaswa kuwasilisha taarifa zake kwa Waziri mwenye dhamana ya masuala ya haki za binadamu
Rais Magufuli awajia juu Waziri na Mwanasheria Mkuu
Rais  Dkt. Magufuli leo Februari 1, 2018 amewabadilikia Waziri wa Katiba na Sheria, Prof. Palamagamba Kabudi na Mwanasheria Mkuu wa serikali, George Masaju kuwa wanakwamisha haki kutendeka kwa watu kutokana na kutofanyia kazi mambo ya msingi.

Magufuli amesema hayo alipokuwa kwenye maadhimisho ya wiki ya sheria na kusema yeye ameubwa kusema ukweli hivyo ataendelea kuusema hata kama kuna watu unawaumiza

"Kinachoshangaza pamoja na hatua nzuri ya Serikali kupeleka 'Legal Aid Act' ya mwaka 2017 na mapendekezo mbalimbali kwa ajili ya kuwasaidia wananchi lakini 'regulation' mpaka saizi hazijaletwa ila Waziri yupo tena Mwanasheria, tena ni Profesa, AG yupo, Deputy AG yupo jamani mtanisamehe sana mimi ndivyo nilivyo nawasema hapa hapa kwa hiyo wewe Profesa Juma na majaji na mahakimu hamna 'Instrument' za kuweza kutoa uamuzi. Wabunge wao wamepitisha sheria, mimi nikaletewa nikasaini lakini regulations mpaka leo miezi tisa imepita"

Magufuli aliendelea kusisitiza kuwa

"Watu wapo wanakula tu mishahara, magari wanayo na viyoyozi vipo ila wananchi wanapata shida na muda mwingine mtasingiziwa mahakama kwamba hamtoi haki kumbe ni Serikali watendaji wake hawatoi haki kwa Watanzania, ndiyo maana nawaambia changamoto zingine zipo ndani ya Serikali lazima na mimi nijitathimini ninachaguaagaje hawa watu ambao wanachelewesha chelewesha, hiyo ndiyo tathimini ambayo ninaanza kujifanyia kuanzia leo"
TFDA yasajili jumla ya vipodozi 3179 vinavyoruhusiwa kuingia nchini

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imesema kuwa TFDA imesajili jumla ya vipodozi 3179 ambavyo vinavyoruhusiwa kuingiza na kutumika nchini.

Akizungumza leo bungeni mjini Dodoma, Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Faustine Ndungulile amesema kuwa katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/217 maeneo 3648 yalikaguliwa ambapo kati ya hayo maeneo 120 yalikutwa na vipodozi ambavyo havina viwango.

“TFDA imekuwa ikichukua hatua zifuatazo kudhibiti uingiaji na utumiaji wa vipodozi. Vipodozi vyote vinatakiwa kusajiliwa kabla ya kibali cha kuingiza nchini kutolewa mpaka sasa TFDA imesajili jumla ya vipodozi 3179 ambavyo ndivyo vinavyoruhusiwa kuingiza na kutumika nchini, TFDA imefungua ofisi 7 za Kanda kwa maana Arusha, Dar es salaam, Dodoma, Mbeya, Mtwara, Mwanza, Tabora kwa lengo la kuimarisha ukaguzi,” amesema Dkt. Ndungulile.

“Katika kipindi cha mwaka wa fedha 2016/017 maeneo 3648 yalikaguliwa ambapo kati ya hayo maeneo 120 yalikutwa na vipodozi ambavyo havina viwango vinavyofaa kwa matumizi ya binadamu na wahusika kuchukuliwa hatua za kisheria.”

Hatua ya ufafanuzi huyo imekuja baada ya Mbunge Mata ally salum Mbunge wa Shauri Moyo aliyeuliza “wananchi wengi hapa nchini hasa wanawake hutumia vipodozi ambavyo havina viwango vinavyofaa kwa matumizi ya binadamu pamoja na jitihada za serikali kuzuia bidhaa hizo Je serikali ina mpango gani madhubuti ya kuzuia vipodozi hivyo.?
Mnyika: "Msaliti huwa haachi usaliti"
John Mnyika.

Mbunge wa Kibamba kupitia Chama cha Kidemokrasia na Maendeleo (CHADEMA) John Mnyika amewatahadharisha wananchi wa jimbo la Kinondoni kwa kutomchagua mgombea wa CCM, Maulid Mtulia kwa madai ni msaliti na hawezi kuacha hiyo tabia.

Mnyika ametoa kauli hiyo ikiwa yupo katika muendelezo wa kumpigia kampeni mgombea wa Ubunge wa jimbo hilo Salum Mwalimu kupitia tiketi ya CHADEMA chini ya mwamvuli wa UKAWA.

"Mtulia alianza usaliti tangu siku ya kwanza alipotangazwa kuwa Mbunge mwaka 2015, maana siku ile matokeo yalipokuwa yanatangazwa na tume, aliposikia jina lake tu kuwa ameshinda alikimbia na kuwaacha watu waliokuwa wakipigania atangazwe na hakutaka kusikia matokeo ya Urais", alisema Mnyika.

Pamoja na hayo, Mnyika aliendelea kwa kusema "msaliti huwa haachi usaliti, hivyo kama wananchi wakikosea na kumpa Mtulia ridhaa ya kuwa Mbunge basi atakuja kuwasaliti tena".

Kwa upande mwingine, mpaka sasa zimebakia takribani siku 16 ili wananchi wa jimbo la Kinondoni  na Siha kuweza kushiriki kupiga kura katika majimbo hayo ambayo yapo wazi kwa sasa.

Mbunge CUF afunguka Wabunge kutelekeza watoto wao
 Mbunge wa Konde (CUF), Khatib Said Haji leo Februari 1, 2018 ameibua tuhuma bungeni, akidai baadhi ya wabunge wenzake wamewatelekeza watoto wao.

Amesema katika mkutano wa Bunge uliopita,  mmoja wa mtoto aliyetelekezwa na wawakilishi hao wa wananchi, aliletwa bungeni na mama yake.

Akizungumza katika kipindi cha maswali na majibu bungeni, Khatibu amesema sasa chanzo cha watoto wa mitaani kimethibitika kwa sababu wanaume wengi wanashindwa kutunza familia zao.

“Mheshimiwa mwenyekiti Bunge lililopita nilishuhudia wanawake wengi wakija na watoto wao pale nje (ya viwanja vya Bunge) wakidai kutelekezwa na wazazi wenzao ambao ni wabunge wanaume. Tabia  hii itakwisha lini na wabunge waanze kutunza watoto wao," amesema Khatibu.

Khatibu ameungwa mkono na mbunge wa Kavuu (CCM), Dk Pudensiana Kikwembe, aliyetaka jambo hilo kuwekwa wazi ili kujua kama wabunge hao wamezaa na wabunge wenzao au wamezaa na watu wengine lengo likiwa ni kujua jinsi ya kuwasaidia.

Katika ufafanuzi wake, Naibu Waziri wa Afya, Dk Faustine Ndugulile amesema kitendo cha kutelekeza watoto ni kinyume na sheria za nchi, kuwataka wananchi, hasa wanaume kuacha tabia hizo.

Hata hivyo, Naibu Waziri huyo amesema Bunge halina taarifa za wabunge kutelekeza watoto..

Kuhusu hoja kama wamezaa na wabunge wenzao ama la, Dk Ndugulile ameomba kiti cha Spika kufuatilia suala hilo kwa maelezo kuwa yeye hawezi kulijibu
Ameishtaki Serikali kwa kumlazimisha kufunga kizazi kwa lazima

Mwanamke mmoja nchini Japan, ambaye alilazimishwa kufungwa kizazi miaka ya 1970 akiwa na umri wa miaka 15, ameishitaki serikali katika kesi ya kwanza ya aina yake.

Mwanamke huyo ambaye hakutajwa jina lake ni mmoja wa wanawake 25,000 waliopitia upasuaji wa kuwafungwa kizazi chini ya sheria ambayo kwa sasa haitekelezwi.

Waathiriwa walifungwa kizazi kwa sababu walibainika kuwa na magonjwa ya kiakili ama wenye matatizo kama vile ukoma.

Mwanamke huyo ambae kwa sasa ana umri wa zaidi ya miaka 60, alichukua hatua ya kisheria baada ya kubaini kuwa alifungwa kizazi chake mwaka 1972 baada ya kupatikana na maradhi ”ya urithi ya kasoro ya ubongo”.

 Taarifa zinasema mwanamke huyo anataka alipwe fidia ya $101,000 (ZAIDI YA TSH. 224.7) kwa uharibifu huo aliotendewa kwenye mwili wake, akielezea
Rais Magufuli atangaza Kiama kwa wanaochelewesha kesi Mahakamani

Dar es Salaam. Rais John Magufuli ametangaza 'kiama' kwa watumishi wa umma ambao wamekuwa wakichelewesha kesi mahakamani hususan wanasheria huku akisisitiza mwezi huu hautaisha atawashughulikia wote kwani anawafahamu.

Pia, Rais Magufuli ametoa mwezi huu kwa Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju kukamilisha kanuni za msaada wa kisheria.

Akizungumza leo Februari mosi, 2018 katika siku ya Sheria, Rais Magufuli amesema usimamizi wa sheria na utoaji wa haki bado una changamoto, wapo wachache uadilifu wao na matendo yao yanachafua vyombo vyeti.

"Wanatoa hukumu zinazopendelea watu, kuchelewesha hukumu au kesi na kati ya 112 waliofukizwa au kustaafishwa 27 walikuwa Mahakimu na wote walipokwenda Mahakamani walishinda," amesema Rais Magufuli na kuongeza,

"Walikuwa Mahakimu 14 walifukuzwa kazi, 67 watumishi wa kawaida walifukuzwa kazi. Wito wangu kwa vyombo vingine IGP, Mkuu wa Magereza, Takukuru muige mfano wa Profesa Juma (Ibrahim Juma-Jaji Mkuu,"
"Majaji mnisamehe. Sitalalamika tena, nishajifunza, najua wapi tunakosea, mwaka jana nililalamika, mwaka huu sitalalamika, najua jinsi ya kufanya na wala mwezi huu hautaisha," amesema Rais Magufuli

Pia, Rais Magufuli amemwagiza Jaji Mkuu, Profesa Juma kupitia Tume ya Utumishi wa Mahakama kufanya uchunguzi kwa baadhi ya majaji ambao wao kila likizo zao wanakwenda mapumziko ulaya jambo linalotia minong'ono ya nani anawagharamikia wakati mishahara yao inajulikana.

Rais Magufuli amewanyooshea vidole Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali, George Masaju, Naibu Mwanasheria Mkuu, Gerson Mdeme wameshindwa kuandaa kanuni za msaada wa kisheria.

"Bunge limepitisha, mimi nimesaini lakini Waziri wa Katiba na Sheria tena Profesa, AG, Naibu AG wote wapo, wanakula mishahara, magari ya kiyoyozi wanayo lakini miezi tisa wameshindwa kuandaa kanuni," amesema Rais Magufuli

"Wakati mwingine na mimi najitathimini nawachaguaje chaguaje hawa. Nataka mwezi huu kanuni ziwe zimekamilika kwani wakati mwingine majaji na Mahakama wanalalamikiwa bure," ameongeza

Rais Magufuli amesema vitendo vya rushwa vipo na "nina taarifa nyingi kweli kweli, rushwa haifichiki na Jaji Mkuu hao majaji wanaokwenda ulaya kufuatilia vibali vyao."

Awali akimkaribisha Rais Magufuli, Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma ameiomba Wizara ya Katiba na Sheria kupitishwa kwa Kanuni ili kuruhusu kuanza kutumika kwa Mahakama inayotembelea ili kusogeza huduma  za kisheria karibuni zaidi.

Amesema umuhimu wa Mahakama lazima upewe kipaumbele na kwa kutumia wiki ya Sheria watafakari walipotoka, walipo na wanapokwenda.

Amesema Mahakama imejiwekea malengo ya kuongeza kasi, uwazi na uadilifu na hawataki kusikia shauri lake lipo wapi na kwa jani yupi au kusikia jalada lake limepotea yote hayo yanaondolewa na mfumo wa Tehama.

"Wananchi wa Tanzania, watarajie huduma bora za uendeshaji wa kesi, uwazi na huona hukumu kwani Tehama itarahisisha yote haya na sisi majaji, mahakimu na watendaji wa Mahakama tubadili fikiri zetu na kuijua Tehama kwani karne hii inahitaji kwenda na wakati," amesema Profesa Juma

Amesema utaratibu unafanyika ili kukamilisha mfumo wa menejimenti za kesi ambayo itatumika kulipa ada, uendeshaji wa kesi kwa masafa ya mbali.

Amesema idadi ya majaji waliopo hayaendani na majalada wanayopewa kuyasikiliza kwani majaji waliopo ni 62 pekee na kila mwaka wanabeba majalada 535 badala ya 225 wanayopaswa kuyasikiliza.

"Huu ni mzigo mkubwa sana na iko nje ya makubaliano kwamba kila jaji amalize majalada 225 lakini kwa idadi hii ni mzigo mkubwa sana," amesema Profesa Juma

Amesema mpaka sasa ni mikoa 14 kati 26 pekee ndizo zenye Mahakama Kuu ambapo alidokeza malengo ni kuwa na Mahakama Kuu katika mikoa 22 ifikapo mwaka 2020.

Jaji Mkuu amesema malengo yao ifikapo mwaka 2020 wilaya zote 139 za Tanzania bara zinakuwa na Mahakama za wilaya.

Amesema katika kipindi cha 2016/17, Tume ya Utumishi wa Mahakama ilisikiliza malalamiko ya kimaadili 143 ambapo kati ya waliofukuzwa au kustaafishwa ni 112 na 17 walirudishwa kazini.

"Hatutamwonea mtumishi lakini hatutamvumilia mtu anayetupaka matope sisi kama Mahakama," amesema Jaji Mkuu

Kwa upande wake, Makamu wa rais wa Chama cha Mawakili Tanganyika (TLS), Godwin Ngwilimi amesema ukiweka pembeni tofauti za kiitikadi, kiongozi anayetuunganisha ni Rais Magufuli.

"Matarajio yake (Rais Magufuli) hayafiki kwetu sisi na kwa maoni yangu matarajio ya kiongozi wangu huyu yanaakisi matarajio ya wananchi," amesema Ngwilimi

Akitoa wito kwa Majaji, Ngwilimi amesema "Mahakama inafaa kuwa mahali iliyotukuka kwani ni mahali pekee tunapokuwa na migogoro, pale tunapoililia sheria tunakwenda mahamakani na hii haijalishi aina ya mtu."

"Tusiitumie Mahakama kama majaribio, maabara au jumba la kamari. Majaji msiitumie hata Mara moja kwani mnalindwa kisheria na msimamie hilo ili Mahakama isionekane ya ajabu ajabu," ameongeza

Naye Naibu Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Gerson Mdeme amesema utoaji haki unahitaji ushirikiano kutoka wa wadau mbalimbali na ofisi ya Mwanasheria Mkuu imekuwa ikifanya hivyo kwa maslahi ya Taifa na wananchi.

Mdeme alitolea mfano kati ya Julai na Desemba mwaka jana iliendesha mashtaka mbalimbali ya jinai yenye thamani ya Sh45 bilioni na dola za Marekani milioni tisa ambazo kama tusingefanya hivyo Serikali ingetakiwa kulipa kiasi hiki cha fedha.

"Kwa utumiaji wa tehama utaongeza utoaji haki kwa haraka na vyombo vingine kama baraza la kata, biashara, mahakama na mengine yanahitaji kuitumia ili kumaliza kesi haraka na kwa wakati

," amesema Mdeme

Amesema ni muhimu kuwa na bajeti na rasilimali watu zinazojitosheleza ili kuhimili matumizi ya Tehama ambayo inaleta mapinduzi makubwa ya utoaji haki.

"Kupungua kwa gharama, kupunguza urasimu, kuwahisha utoaji wa haki na watumishi wasio waaminifu mfumo huu wa Tehama utawaumbua kwani shughuli zitafanyika kwa uwazi," amesema Mdeme

"Tumejiandaaje na wizi wa mitandao, watu wetu wameandaliwa kiasi gani katika matumizi ya Tehama, tumejiandaaje kuweka mazingira salama kwa maslahi ya Watanzania," ameongeza

Siku hiyo ya sheria yenye kauli mbiu 'Matumizi ya Tehama katika utoaji haki na kwa wakati' ilitanguliwa na maombi yaliyotolewa na viongozi mbalimbali wa dini walioombea Serikali, Mahakama na Bunge.

Amesema angefurahi  kuona IGP naye anatoa majina ya polisi wanaochelewesha upelelezi hata kama mtu kashikwa na dawa za kulevya au mkuu wa magereza watu wanaoingiza simu gerezani.

Ridhiwani atoa agizo afisa mtendaji kuondolewa mara moja

Chalinze. Mbunge wa Chalinze (CCM), Ridhiwani Kikwete ametaka kuondolewa mara moja kwa ofisa mtendaji wa kata ya Vigwaza, Elizabeth Msenga kwa maelezo kuwa ameshindwa kutekeleza majukumu yake ipasavyo.

Ridhiwani ametoa kauli hiyo leo Februari1, 2018 katika mkutano wa hadhara uliofanyika kijijini humo, kutaka mtendaji huyo kupangiwa eneo jingine la kazi.

Amesema haiwezekani wananchi wanapata matatizo na kukosa mtu wa kuwasikiliza na kuwasilisha kero zao sehemu husika.

“Yaani akija mbunge ndio wananchi wanalalamika jukwaani. Uzembe huu unasababisha wananchi kuwa na hasira na kukichukia CCM wakidhani hakiwasilizi na hakiwajali kumbe ni uzembe wa mtu mmoja tu,” amesema na kuongeza,

"Nimezunguka vijiji zaidi ya vinne kero zinazopewa ni nyingi lakini utatuzi wake upo chini ya Serikali ya kata. Nashangaa hata ofisa mtendaji hayupo katika ziara na si mara ya kwanza, hakuna taarifa ya Serikali iliyoandaliwa.”

Wakati ombi lake la kutaka ofisa huyo kuondolewa likishangiliwa na wananchi waliohudhuria mkutano huo uliokuwa sehemu ya ziara ya mbunge huyo kukagua miradi ya maendeleo, mwenyekiti wa CCM kata ya Vigwaza, Shedeli Mikole amesema hali hiyo inatokana na viongozi kufanya kazi kwa mazoea.

“Ombi lako litafanyiwa kazi kwa sababu Vigwaza kuna tatizo kubwa la utekelezaji wa shughuli za maendeleo,” amesema.

"Mbunge nikuhakikishie hoja hii itafanyiwa kazi na sio siri hapa Vigwaza kuna tatizo la kasi ya utekelezaji shughuli za maendeleo. Huyu mjini hawezi kabisa tumeshamuona siku nyingi anapaswa aende kata nyingine pembezoni mwa mji, "amesema Mikole.

Hata hivyo,  Msenga alipotafutwa kwa njia ya simu na Mwananchi amesema hakuweza kuhudhuria ziara hiyo kwa kuwa ni mgonjwa.