FAMILIA ya Mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha Usafirishaji (NIT), Akwilina Maftah (22), ambaye alifariki kwa kupigwa risasi na polisi Ijumaa iliyopita, imeandaa bajeti ya Sh. milioni 80 ya mazishi yake, lakini serikalini imesema itakaa na ndugu hao kujiridhisha.
Akwilina alifariki baada ya kupigwa risasi akiwa ndani ya daladala eneo la Mkwajuni, Kinondoni na polisi waliokuwa wakijaribu kutawanya maandamanao ya wafuasi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Ijumaa jioni.
Baada ya kifo hicho, serikali iliahidi kugharamia mazishi na juzi kikao cha msiba huo, pamoja na mambo mengine, kiliandaa bajeti ya Sh. milioni 80 ambayo ilikabidhiwa serikalini jana.
Msemaji wa familia hiyo, Festo Kavishe, aliliambia Nipashe kuwa baada ya kuikabidhi, walitaraji kukutana na wawakilishi wa serikali kwa ajili ya kuichanganua.
Lakini akizungumza na Nipashe kwa njia ya simu jana, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako alisema wamepokea mapendekezo hayo na kwamba walitarajia kukaa na familia "jioni" kwa ajili ya kuipitia, ili kujua uhalisia wake.
"Ni kweli wametupa mapendekezo yetu, lakini serikali ina utaratibu wake," alisema Prof. Ndaliachako. "Katibu Mkuu wangu ameyapokea mapendekezo hayo na watakaa jioni ili kupitia kipengele kwa kipengele."
Alisema serikali iliipa uhuru familia hiyo kufanya maandalizi na kuandaa mapendekezo, ikiwamo bajeti ya mazishi hayo, kwasababu iliona si busara kuwaingilia.
"Tutakaa kuiangalia ili kujiridhisha na uhalisia wa mapendekezo yao kwa sababu serikali ina utaratibu wake."
Awali Kavishe alisema bajeti waliyoiandaa inaonyesha jeneza la marehemu litanunuliwa kwa Sh. milioni 1.5, malipo ya hospitali Sh. 200,000, gari la kubeba mwili Sh. milioni tatu, magari ya msafara makubwa matano kwa jumla ya Sh. milioni 20 na chakula cha njiani kwa wasafiri Sh. milioni tatu.
Aidha, bajeti hiyo inaonyesha bajeti ya chakula kwa siku tatu msibani Mbezi mkoa wa Dar es Salaam kuanzia asubuhi hadi jioni ni Sh. milioni 10.
"Mahitaji mengine ni viti 200 kwa gharama ya Sh. 400,000, turubai tatu kwa gharama ya Sh. 600,000, fedha ya muziki na kumlipa mshereheshaji Sh. 400,000 picha za kumbukumbu Sh. milioni moja na maji ya kunywa Sh. 50,000," alisema.
Kavishe alisema kamati imeandaa bajeti nyingine ya siku tano ambayo itatumika kwenye shughuli ya mazishi Rombo mkoani Kilimanjaro ambapo gharama ya chakula kwa siku zote ni Sh. milioni 30.
Alisema muziki na mshereheshaji kwa siku zote tano ni Sh. milioni mbili, maturubai manne kwa gharama ya Sh. milioni moja, viti 400,000 na kaburi la kisasa Sh. milioni tatu.
"Maua na mataji tumeweka Sh. milioni moja, mapambo Sh. 500,000 na dharura Sh. milioni mbili," alisema zaidi Kavishe na kwamba "kwa ujumla bajeti nzima ya shughuli hii kwa siku nane itakuwa ni Sh. milioni 80."
HATUA ZA KISHERIARais John Magufuli alisema katika akaunti yake ya mtandao wa kijamii ya Twitter Jumapili "Nimeviagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi na kuwachukulia hatua za kisheria waliosababisha tukio hili."Rais Magufuli pia alielezea kusikitishwa "sana" na kifo cha Akwilina, na kutoa pole kwa familia, ndugu, wanafunzi wa NIT na wote walioguswa na msiba huo.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam siku hiyo pia, Waziri Ndalichako alisema Akwilina alikuwa mwaka wa kwanza wa Shahada ya Ununuzi na Ugavi katika chuo hicho.
"Wizara yangu itagharamia mazishi yake hadi hapo atakapopumzishwa katika makao yake ya milele," alisema Prof. Ndalichako. "Tutasimamia shughuli zote za msiba huo.
"Tunatoa pole kwa ndugu, jamaa na marafiki... kwa uongozi wa NIT, kwa wanafunzi na wananchi wote."Serikali imepata pigo kubwa kwa sababu inawekeza pesa nyingi katika kuwasomesha wanafunzi kuanzia elimu ya msingi hadi elimu ya juu kwa kuwapa mikopo."
Aidha, Prof. Ndalichako alisema siku ya Ijumaa Akwilina alikuwa njiani kupeleka barua ya kuomba kufanya kazi kwa vitendo katika moja ya kampuni zilizopo Bagamoyo mkoa wa Pwani.
Marehemu alipanda daladala linalofanya safari kati ya Mabibo na Makumbusho katika kituo cha NIT na kufuatia maelezo ya waziri kwamba alikuwa akielekea Bagamoyo, ilikuwa ashuke mwisho wa safari kabla ya kuunganisha daladala nyingine kwenda Bunju Sokoni au Tegeta Nyuki zilizo stendi za Bagamoyo.
Taarifa za kipolisi zilizotolewa mwishoni mwa wiki iliyopita zilisema mwili wa marehemu aliyekuwa amekaa kiti cha nyuma katika daladala hiyo yenye namba T558 CSX aina ya Nissan Civilian, ulikutwa ukiwa na jeraha kubwa kichwani lililoonekana kutokana na kupigwa na kitu chenye ncha kali, kilichoingia upande wa kulia na kutoka upande wa kushoto.