KAMPALA, UGANDA: Mkataba wa mradi wa Bomba la Mafuta kati ya Tanzania na Uganda(Intergovernmental Agreement - IGA) umesainiwa leo.
Ujenzi wa bomba hilo la kutoka Hoima nchini Uganda hadi Tanga nchini Tanzania lenye urefu wa Kilometa 1,443, uliokadiriwa kugharimu zaidi ya Dola bilioni 3 nukta 55.
Tukio hilo limekuja siku chache baada ya Marais wa Nchi hizo mbili, Dkt. John Pombe Magufuli na Rais wa Jamhuri ya Uganda Yoweri Kaguta Museveni, kutia saini tamko la pamoja la kukamilika kwa majadiliano ya vipengele vya mkataba, Ikulu Jijini Dar es salaam.
Hafla ya kutia saini Mkataba huo iliyofanyika katika Hoteli ya Serena, Jijini Kampala, Uganda imehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa nchi zote mbili wakiwemo Mawaziri, Makatibu Wakuu, Wanasheria Wakuu wa Serikali, Wakurugenzi na Viongozi wa taasisi mbalimbali zinazohusika katika mradi huo.
Mradi wa Bomba la Mafuta Ghafi kutoka Hoima-Uganda hadi Tanga Tanzania, unatarajia kusisimua uchumi wa nchi hizo mbili na katika mchakato wa ujenzi wake zaidi ya watu 10,000 wanatarajiwa kunufaika na ajira.
Hivi Karibuni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli aliuelezea mradi huo kuwa ni mkubwa kwakuwa Uganda imegundua shehena kubwa ya mafuta katika eneo la Hoima kiasi cha mapipa bilioni 6 na laki 5 na kwamba Tanzania inatarajia pia kupata mafuta kule ziwa Tanganyika na ziwa Eyasi, ambayo yatapitishwa katika bomba hilo hilo.